BUGANDO MEDICAL CENTRE

Consultant and Teaching Hospital for the Lake and Western zones of the United Republic of Tanzania

::Bugando Medical Centre
ASBAHT YA ZINDIUA TAWI JIPYA MWANZA

Chama cha Wazazi wenye Watoto wa Kichwa Kikubwa na Mgongo Wazi Tanzania (ASBAHT), kimezindua rasmi tawi jingine katika mkoa wa mwanza. Uzinduzi huo ulifanyika katika Hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza na Mwakilishi wa mganga mkuu wa Mkoa Bw Tuloson Nyalaja, mfamasia wa mkoa.

Chama hiki chenye lengo la kueneza elimu juu ya tatizo hili ambalo limeendelea kujitokeza kwa kasi nchini na bado jamii haijajua nini chanzo cha tatizo hili. Kulingana na takwimu zinavyoonyesha watoto wenye matatizo hayo yanazidi kuongezeka siku hadi siku, hivyo chama hiki kimekuja na dhamira ya kueneza elimu juu ya kinga, tiba ya mapema na malezi bora, kushawishwi na kutetea haki za watoto katika ushirikishwaji kijamii, kielimu, kazi za mikono na kuwezeshwa kiuchumi.

Tangu chama hiki kianzishwe kimefanikiwa kuwaleta wazazi pamoja, watoto wameweza kupata huduma ya vipimo katika hospitali za binafsi, mfano CT-SCAN, pamoja na mafanikio hayo , wanakabiriana na changamoto kama vile ukosefu wa tiba hiyo mikoani, wazazi kutokuwa na elimu juu ya ugonjwa huo, ukosefu wa shant, gharama za vipimo kuwa kubwa, wazazi wa kiume kukimbia familia zao wakiwa na imani kuwa ni mkosi au balaa katika familia yake, wazazi kukata tama juu ya matumaini ya kukua mtoto wao na kukosa ushauri wa jinsi ya kuwahudumia watoto baada ya kupata upasuaji.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya katika Hospitali ya Bugando Dr. Alfonce Chandika amesema , tatizo hili limekuwa likiongezeka siku hadi siku, kwani watoto wengi wenye tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi wamekuwa wakifika hospitalini wamechelewa na kufanya tatizo kuwa zaidi.

Ameongeza kusema , jamii ijue ni tatizo linaloletwa na matatizo mbalimbali na wala sio imani potofu kwani tatizo hili likifanyiwa uchunguzi mapema na kupata matibabu mtoto anapona. Amesema katika hospitali ya Bugando kulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa mipira kwa ajiri ya kuwawekea watoto kwajili ya kutolea maji,lakini kupitia shirika la ASBAHT limefanikisha hilo kwa kutumia wahisani mbalimbali na amesema kwa hapa Bugando tayari tunaye Daktari Bingwa kwa ajili ya tatizo hilo ambaye ni Dr. E.Saguda na mwingine bado yupo masomoni, amesema.

Naye mwakilishi wa Mganga mkuu wa mkoa Bw. Tuloson Nyalaja Mfamasia wa Mkoa, Amesema elimu ya kutumia dawa za folic Acid miezi mitatu (3) kabla ya kubeba ujauzito itolewe kwa jamii kwani ni tatizo ambalo linaweza epukika, ameongeza kuwa mkoa wa Mwanza utaliweka hili katika mikakati yake.

Chama cha wazazi wa watoto wenye kichwa kikubwa kilianzishwa mwaka 2001 na kusajiriwa mwaka 2008 mpaka sasa kina wanachama mia nne (400) na matawi manane (8) ambayo ni Morogoro, Tanga,Dodoma, Musoma, Moshi, Arusha, Dar es salaam, Mbeya na sasa Mwanza.